SIKU moja baada ya majibizano ya risasi kati ya askari na watu
wanaodaiwa kuwa ni majambazi katika eneo la Vikindu wilaya ya Mkuranga
katika mkoa wa Pwani, Jeshi la Polisi limetuma kikosi cha askari zaidi
ya 80 kwenye operesheni maalumu katika maeneo ya Vikindu, Mkuranga na
jirani kuwasaka majambazi.
Katika mapambano hayo yaliyodumu kwa saa saba katika Mtaa wa Vikindu Mashariki, Mkuranga, askari mmoja alipoteza maisha.
Akizungumzia operesheni inayoendelea ya kupambana na uhalifu katika
maeneo hayo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon
Sirro alisema operesheni hiyo ilianza tangu Alhamisi baada ya mauaji ya
askari wanne waliokuwa wakilinda katika benki ya CRDB iliyopo Mbande
katika Manispaa ya Temeke.
Alisema wamekuwa wakipokea taarifa nyingi kutoka kwa raia wema na
wamezifanyia kazi, ikiwa ni pamoja na operesheni hiyo ya Vikindu ambayo
imefanikisha kukamatwa kwa watu kadhaa na wengine kuuawa.
Kamishna Sirro alikataa kutaja idadi ya watu waliouawa na
waliokamatwa, kwa madai kuwa operesheni hiyo inaendelea hivyo kutaja
idadi yao ni sawa na kuvuruga utaratibu wa operesheni hiyo.
“Operesheni ninaposema sasa inaendelea mkiangalia pale chini kuna
askari zaidi ya 80 wanaendelea kwenye misitu hiyo, kwa hiyo ninaposema
operesheni inaendelea siwezi kusema nani kapata nini kwa wakati gani,
naomba waandishi wa habari mnivumilie,” alisema Kamishna Sirro.
Alisema itakuwa ni jambo la kinyume cha taratibu za kazi kuwa kwenye
operesheni huku akitoa taarifa, na kwamba operesheni hiyo imeanza tangu
Alhamisi na kuahidi hadi kufikia Jumanne atakuwa na taarifa kamili
kuhusu operesheni hiyo na ataitisha mkutano mwingine wa wanahabari ili
kuwapa taarifa kamili.
Alisema kubwa zaidi wana Dar es Salaam, wanahitaji kuona silaha
zilizoporwa kwa askari hao waliouawa zinarudi, ambapo alisema kutokana
na msako huo silaha hizo zitarudi. “…Kuna mawili, unapoua unategemea
nini, kwa hiyo kimsingi operesheni inaendelea vizuri kuna watu kadhaa
wameuawa na watu kadhaa wamekamatwa, lakini nitawajulisha Jumanne kitu
gani kimefanyika,” aliongeza.
Akijibu swali kuhusu ukubwa wa mapambano hayo hadi kutumwa kwa kikosi
kikubwa cha askari wenye silaha, alisema mapambano yaliyoko huko ni ya
kawaida, hasa kwa kuzingatia kwao mapambano ya silaha ni jambo la
kawaida sana na hata kufa kwao kwa bunduki ni kawaida, kwa kuwa waliapa
kufa kwa ajili ya hilo.
Operesheni hiyo itafanyika katika maeneo mbalimbali ya Vikindu,
Pwani, Dar es Salaam na mikoa ya jirani kwa kuwa mtandao huo bado na
kusisitiza kuwa Dar es Salaam ilizoea kuwa shwari hivyo ni lazima
heshima yake irudi.
Tukio la kuuawa kwa askari mmoja katika tukio la Vikindu linafanya
idadi ya askari waliouawa ndani ya wiki hii kufikia watano wakiwamo
wanne waliouawa wakati wakipokezana lindo katika benki ya CRDB iliyopo
Mbande, Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Vikindu Mashariki,
Mohammed Maundu amekiri hakuwa na taarifa za kuishi na majambazi katika
eneo lake mpaka aliposikia mirindimo ya risasi usiku wa Alhamisi.
Aliifahamu nyumba waliokuwa wakiishi watuhumiwa hao waliokaa eneo hilo
kwa muda wa miezi 36, lakini hakuwafahamu wapangaji wala mipango yao.
“Nakiri watu hawa waliishi katika eneo langu lakini sikuwafahamu.”
Maundu alisisitiza Vikindu ni eneo linaloongezeka kwa haraka lakini ni
vigumu kufahamu kila mtu anayeishi au kutembelea eneo hilo. Mkazi mmoja
wa eneo hilo, anayemiliki duka kijijini hapo alitoa maoni tofauti,
akisema watu hao walikuwa wateja wake wa kila siku lakini hakuwahi
kuhisi kuwa wana malengo mabaya zaidi ya kuwaona kama marafiki.
Hata hivyo, mkazi huyo alikiri kuwa eneo hilo limekuwa na matukio ya
uporaji wa mara kwa mara kwa sababu kijiji hicho kipo karibu na msitu wa
Kongowe.
Inadaiwa kuwa msitu wa Kongowe ni makazi ya wahalifu. Chanzo cha
kuaminika kilidai kuwa makundi ya wahalifu ambayo yako katika operesheni
maalumu ya kulipiza visasi yamekuwa yakijificha katika msitu wa
Mkuranga.
Mkazi mwingine anayeishi nyumba ya karibu, Rukia Mnende, alisema
anamfahamu mmiliki wa nyumba waliokuwa wakiishi watuhumiwa hao wa
ujambazi.
Alifafanua kuwa mmiliki wa nyumba alihamia wilaya ya Temeke, lakini
hakuwafahamu waliopanga katika nyumba hiyo pamoja na kuishi katika
nyumba hiyo miaka mitatu mpaka Ijumaa, yalipotokea mapigano kati ya
polisi na watu hao.
Salum Mpili alisema watuhumiwa walikuwa wakitoka majira ya usiku tu,
hivyo ilikuwa vigumu kuwafahamu. Tukio la juzi limewaacha bado wakazi wa
eneo hilo katika hali ya hofu kubwa. Huku baadhi yao wakitaka vyombo
vya dola kufanya upekuzi wa kina kuwafichua wahalifu zaidi ambao
walikuwa wanageuza eneo hilo maficho yao