Sunday, 28 August 2016

Zanzibar yaaga kishujaa – Mashindano ya Chalenji


Awassa. Ethiopia. Zanzibar Heroes ikiwa katika ubora wake ilikumbuka shuka kukiwa kumekucha baada ya kuikamua Harambee Stars ya Kenya kwa mabao 3-1 katika pambano la kukamilishia ratiba la Kombe la Chalenji.
Wakati Zanzibar Heroes wakikamilisha ratiba kwa ushindi huo mnono, ndugu zao, Kilimanjaro Stars leo wataikabili Ethiopia katika mchezo ambao ni kama wa kukamilisha ratiba kwani tayari Kili Stars imefuzu hatua ya robo fainali.
Kiwango walichokionyesha Zanzibar jana ni tofauti na michezo yao miwili iliyopita dhidi ya Burundi na Uganda, ingawa ni kudra za Mwenyezi Mungu ndizo zitawavusha na kucheza robo fainali kama mshindwa bora (best loser) wakitegemea matokeo baina ya Uganda na Burundi zitakazocheza leo.
Hata hivyo, kocha mkuu wa Zanzibar Heroes, Hemed Morocco alisema ni kama hawana nafasi tena katika mashindano hayo, lakini amewapongeza wachezaji wake kwa kutolewa mashindanoni kishujaa baada ya kupata ushindi mkubwa.
“Ingawa itategemea na matokeo ya kesho(leo) katika Uganda na Burundi, lakini niseme tumeshatolewa, nawasifu wachezaji wangu wametoka kishujaa kwa kucheza na kupata ushindi mbele ya Kenya, “alisema Morocco.
Katika mchezo huo, mabao mawili kutoka kwa Suleiman Kassim ‘Selembe’ (pichani) na Mcha Khamis yalitosha kuipa Heroes ushindi huo wa kwanza wa kundi B, lakini ikiwa haina uhakika wa kupita katika kapu ya mshindwa bora ili kufuzu kucheza robo fainali.
Kenya ikiongoza msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi nne sawa na Burundi itakayoumana na Uganda leo, iliingia Uwanja wa Taifa wa Ethiopia mjini hapa ikiwaacha nyota wake wengi nje na Zanzibar ilitumia mwanya huo kuiadhiri.
Selembe alifunga bao la kwanza dakika moja kabla ya mapumziko kabla ya kupiga krosi tamu katika dakika ya 57 iliyounganishwa vema kimiani na Mcha Khamis na kuiandikia Zanzibar bao la pili.
Wakati Harambee ikitafuta mbinu za kurejesha mabao hayo, Selembe tena aliichambua safu ya ulinzi ya Kenya kabla ya kumtungua kipa wa timu hiyo kuandika bao la tatu wakati Kenya walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Jacob Keli, dakika ya 90.
Kutokana na matokeo hayo, Zanzibar Heroes ina pointi tatu sawa na Uganda na Ethiopia, ingawa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa unaiweka Heroes katika nafasi ngumu ya kusonga mbele kama mshindwa bora.
Kilimanjaro Stars leo itawakabili wenyeji Ethiopia, lakini ikihitaji kushinda ili kuendelea kuongoza kundi lao.
Kocha mkuu wa kikosi hicho, Abdallah ‘King’ Kibadeni alisema licha ya kuwa wamefuzu, lakini mchezo wa leo lazima washinde ili kuendelea kuweka rekodi katika mashindano hayo.
Kili Stars imeshinda michezo miwili dhidi ya Somalia na Rwanda na inaongoza Kundi A.
“Tumekuja kwenye mashindano, hivyo hatutamwonea huruma yoyote, tunataka kushinda kila mchezo hadi tufike fainali na kuchukua ubingwa kwani Watanzania wametutuma ubingwa na si vinginevyo,” alisema Kibadeni.
Matokea mengine jana, Sudan Kusini iliichapa Malawi, timu mwalikwa mabao 2-0, wakati Sudan ikipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Djibouti ambayo kama Somalia imeaga bila ushindi wowote

1 comment:

  1. Harrah's Philadelphia Casino & Racetrack - Joliet
    Harrah's 거제 출장마사지 Philadelphia Casino & Racetrack is located 인천광역 출장샵 in Joliet, IL 경상남도 출장샵 and features slot machines, 밀양 출장마사지 table games and a wide range 익산 출장안마 of entertainment.

    ReplyDelete