SIKU moja baada ya majibizano ya risasi kati ya askari na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi katika eneo la Vikindu wilaya ya Mkuranga katika mkoa wa Pwani, Jeshi la Polisi limetuma kikosi cha askari zaidi ya 80 kwenye operesheni maalumu katika maeneo ya Vikindu, Mkuranga na jirani kuwasaka majambazi.
Katika mapambano hayo yaliyodumu kwa saa saba katika Mtaa wa Vikindu Mashariki, Mkuranga, askari mmoja alipoteza maisha.
Akizungumzia operesheni inayoendelea ya kupambana na uhalifu katika maeneo hayo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema operesheni hiyo ilianza tangu Alhamisi baada ya mauaji ya askari wanne waliokuwa wakilinda katika benki ya CRDB iliyopo Mbande katika Manispaa ya Temeke.
Alisema wamekuwa wakipokea taarifa nyingi kutoka kwa raia wema na wamezifanyia kazi, ikiwa ni pamoja na operesheni hiyo ya Vikindu ambayo imefanikisha kukamatwa kwa watu kadhaa na wengine kuuawa.
Kamishna Sirro alikataa kutaja idadi ya watu waliouawa na waliokamatwa, kwa madai kuwa operesheni hiyo inaendelea hivyo kutaja idadi yao ni sawa na kuvuruga utaratibu wa operesheni hiyo.
“Operesheni ninaposema sasa inaendelea mkiangalia pale chini kuna askari zaidi ya 80 wanaendelea kwenye misitu hiyo, kwa hiyo ninaposema operesheni inaendelea siwezi kusema nani kapata nini kwa wakati gani, naomba waandishi wa habari mnivumilie,” alisema Kamishna Sirro.
Alisema itakuwa ni jambo la kinyume cha taratibu za kazi kuwa kwenye operesheni huku akitoa taarifa, na kwamba operesheni hiyo imeanza tangu Alhamisi na kuahidi hadi kufikia Jumanne atakuwa na taarifa kamili kuhusu operesheni hiyo na ataitisha mkutano mwingine wa wanahabari ili kuwapa taarifa kamili.
Alisema kubwa zaidi wana Dar es Salaam, wanahitaji kuona silaha zilizoporwa kwa askari hao waliouawa zinarudi, ambapo alisema kutokana na msako huo silaha hizo zitarudi. “…Kuna mawili, unapoua unategemea nini, kwa hiyo kimsingi operesheni inaendelea vizuri kuna watu kadhaa wameuawa na watu kadhaa wamekamatwa, lakini nitawajulisha Jumanne kitu gani kimefanyika,” aliongeza.
Akijibu swali kuhusu ukubwa wa mapambano hayo hadi kutumwa kwa kikosi kikubwa cha askari wenye silaha, alisema mapambano yaliyoko huko ni ya kawaida, hasa kwa kuzingatia kwao mapambano ya silaha ni jambo la kawaida sana na hata kufa kwao kwa bunduki ni kawaida, kwa kuwa waliapa kufa kwa ajili ya hilo.
Operesheni hiyo itafanyika katika maeneo mbalimbali ya Vikindu, Pwani, Dar es Salaam na mikoa ya jirani kwa kuwa mtandao huo bado na kusisitiza kuwa Dar es Salaam ilizoea kuwa shwari hivyo ni lazima heshima yake irudi.
Tukio la kuuawa kwa askari mmoja katika tukio la Vikindu linafanya idadi ya askari waliouawa ndani ya wiki hii kufikia watano wakiwamo wanne waliouawa wakati wakipokezana lindo katika benki ya CRDB iliyopo Mbande, Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Vikindu Mashariki, Mohammed Maundu amekiri hakuwa na taarifa za kuishi na majambazi katika eneo lake mpaka aliposikia mirindimo ya risasi usiku wa Alhamisi. Aliifahamu nyumba waliokuwa wakiishi watuhumiwa hao waliokaa eneo hilo kwa muda wa miezi 36, lakini hakuwafahamu wapangaji wala mipango yao.
“Nakiri watu hawa waliishi katika eneo langu lakini sikuwafahamu.” Maundu alisisitiza Vikindu ni eneo linaloongezeka kwa haraka lakini ni vigumu kufahamu kila mtu anayeishi au kutembelea eneo hilo. Mkazi mmoja wa eneo hilo, anayemiliki duka kijijini hapo alitoa maoni tofauti, akisema watu hao walikuwa wateja wake wa kila siku lakini hakuwahi kuhisi kuwa wana malengo mabaya zaidi ya kuwaona kama marafiki.
Hata hivyo, mkazi huyo alikiri kuwa eneo hilo limekuwa na matukio ya uporaji wa mara kwa mara kwa sababu kijiji hicho kipo karibu na msitu wa Kongowe.
Inadaiwa kuwa msitu wa Kongowe ni makazi ya wahalifu. Chanzo cha kuaminika kilidai kuwa makundi ya wahalifu ambayo yako katika operesheni maalumu ya kulipiza visasi yamekuwa yakijificha katika msitu wa Mkuranga.
Mkazi mwingine anayeishi nyumba ya karibu, Rukia Mnende, alisema anamfahamu mmiliki wa nyumba waliokuwa wakiishi watuhumiwa hao wa ujambazi.
Alifafanua kuwa mmiliki wa nyumba alihamia wilaya ya Temeke, lakini hakuwafahamu waliopanga katika nyumba hiyo pamoja na kuishi katika nyumba hiyo miaka mitatu mpaka Ijumaa, yalipotokea mapigano kati ya polisi na watu hao.
Salum Mpili alisema watuhumiwa walikuwa wakitoka majira ya usiku tu, hivyo ilikuwa vigumu kuwafahamu. Tukio la juzi limewaacha bado wakazi wa eneo hilo katika hali ya hofu kubwa. Huku baadhi yao wakitaka vyombo vya dola kufanya upekuzi wa kina kuwafichua wahalifu zaidi ambao walikuwa wanageuza eneo hilo maficho yao

Post a Comment

 
Top