Serikali imepiga marufuku utaratibu wa shule binafsi kuendesha mitihani
ya mchujo kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya kitaifa ili
shule zao ziweze kuongoza kwa kubaki ma wanafunzi wazuri(walio na uwezo
mzuri darasani)
Agizo hilo pia linapiga marufuku kuwafukuza shule wanafunzi wanaoshindwa
mitihani ya mchujo,kuwasajili kama private candidate wale wanafunzi
wanaofeli mitihani hiyo,kuwahamisha shule au kuwakaririsha madarasa.
Kibano kipya chaja kwa shule binafsi.
Hiyo ni baada ya kutangaza kupiga marufuku utaratibu wa kuwachuja
wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani ya taifa uliokuwa unaofanywa na
baadhi yao kwa lengo la kuonekana shule zao zinafaulisha vizuri.
Hivi karibuni, Nipashe iliripoti kuhusu hofu ya baadhi ya shule hizo; za
msingi na sekondari ziko hatarini kubadilishwa matumizi kutokana na
kukosa wanafunzi wa kutosha baada ya Serikali kuboresha shule zake na
kutoa elimu bure, huku hali ya kiuchumi ikiwaumiza wananchi.
Huku udahili kwenye shule za serikali ukiongezeka na kuonekana kuwa
tishio kwa ustawi wa shule za watu na taasisi binafsi, imewabana tena
wamiliki wa shule binafsi kwa kuwazuia kufanya mchujo wa wanafunzi
wanaoingia kwenye madarasa au vidato vyenye mitihani ya taifa.
Mmoja wa wazazi aliliambia Nipashe kuwa mwanawe anayesoma kidato cha
tatu katika shule moja ya binafsi jijini Dar es Salaam, amepangiwa
kuhamishiwa shule nyingine ya mmiliki huyo huyo kutokana na kufaulu kwa
daraja la tatu.
Kwa mujibu wa mzazi huyo, kuna wanafunzi takribani 70 wa kidato cha
tatu, wanatarajiwa kuhamishwa katika shule hiyo waliyosajiliwa tangu
kidato cha kwanza, watahamishwa shule hiyo na kubaki wale waliofaulu kwa
viwango vya madaraja ya kwanza na pili tu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard
Akwilapo, akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, alisema ni
marufuku shule kumkaririsha darasa, kumfukuza, kumhamishia shule
nyingine au kumsajili kama mtahiniwa binafsi (PC) mwanafunzi kwa kigezo
cha kutofanya vizuri katika mitihani ya shule husika.
"Ni marufuku kabisa kufanya hivyo. Mitihani tulionayo sisi (Wizara ya
Elimu) ndiyo mchujo sahihi. Na mtihani ambao unamkaririsha mwanafunzi ni
mtihani wa taifa wa kidato cha pili na mtihani wa darasa la nne tu,"
alisema.
"Wala siyo mtihani wa shule na madarasa mengine hayana mtihani wa
kumkaririsha mtoto au kumfanya aondolewe shuleni au ahamishiwe shule
nyingine, hatuna utaratibu huo na serikali haiwezi kukubaliana nao,"
aliongeza Dk. Akwilapo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongosco),
Benjamin Nkonye, aliiambia Nipashe jana kuwa utaratibu wanaoutumia ni
kushauriana na wazazi wa wanafunzi wanaoshindwa kufanya vizuri shuleni
ikiwamo kuwapeleka katika vyuo vya ufundi (Veta).
Alisema shule binafsi zinapaswa kupongezwa kwa kudahili hata wanafunzi
hasa wa sekondari ambao shule za serikali huwa haziwachukui kutokana na
kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya shule za msingi.
“Hakuna shule ambazo zinapaswa kupongezwa kama za binafsi, serikali
yenyewe imekuwa ikichagua wanafunzi wote. Inatuachia ‘vilaza’, lakini
sisi kwa kujitoa kuwasaidia watoto wa Kitanzania, tunakubali kuwachukua
hao hao wanaoonekana wabaya, tunawafundisha na mwisho wa siku wanakuwa
wazuri kuliko hata hao wanaokuwa wamethaminiwa na serikali,” alisema
Nkonya.
“Na sisi hatuchuji wala kumfukuza mwanafunzi, isipokuwa kinachofanyika
kwa kuwa tunapokea wakati mwingine wanafunzi ambao ni ‘vilaza’ kabisa,
huwa tunawagawanya katika makundi kulingana na uelewa wao, wenye uelewa
wa kwanza, wa kati na wa mwisho. Na mwisho na tunawafundisha kulingana
na ‘speed’ (kasi) ya uelewa wao na wanajikuta wanafanya vizuri.
“Lakini kwa sababu sisi tunakuwa na wanafunzi ambao ni wagumu sana,
inapoonekana wakatokea wachache hawawezi kabisa huwa tunashauriana na
wazazi wao, kuwapeleka Veta ili kule wanapokuwa wanaendelea kujifunza,
wengine wanafanya vizuri hadi wanafika vyuo vikuu, hatuwaachi kama
ilivyo katika shule za serikali na vyuo vya serikali, haya maneno
mengine yanayozungumzwa ni ya kisiasa tu."
HALI ILIVYO
Uchunguzi wa Nipashe uliofanyika hivi karibuni katika baadhi ya mikoa,
ulibaini baadhi ya wamiliki wa shule binafsi wamekuwa na utaratibu wa
kuchuja wanafunzi kila mwaka kwa lengo la kupata wenye uwezo mkubwa
darasani.
Ilibainika kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanywa kwa nia ya kuwa na
wanafunzi wenye uwezo mkubwa ili shule hizo zifanye vizuri katika
mitihani ya taifa, hivyo kuvutia wazazi wengi zaidi kupeleka watoto wao.
Gazeti hili lilibaini kuwa, baadhi ya shule binafsi zimekuwa zikiendesha
utaratibu huo kipindi cha mitihani ya mwishoni mwa mwaka kwa
kuwafukuza, kuwakaririsha darasa au kuwahamishia shule nyingine
wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango kinachowekwa na shule husika
kwenye mitihani ya kufunga mwaka.
Nipashe pia ilibaini baadhi ya shule hizo zimekuwa na utaratibu wa
kuwachuja kwa kuwasajili kama watahiniwa binafsi (Private Candidates)
kwenye mitihani ya taifa wanafunzi wake wanaoshindwa kiwango
kilichowekwa wanapofanya mitihani ya shule husika.
MTOTO WA PROFESA AKACHA KULA
Akizungumzia suala hilo katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini
Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masomo ya Shahada ya Kwanza Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Allen Mushi, alisema haungi mkono
utaratibu wa baadhi ya shule binafsi kuwafukuza wanafunzi wanaoshindwa
kufikia kiwango cha alama zilizojiwekea.
Alisema: "Ni makosa kumfukuza shule mwanafunzi aliyekuwa amedahiliwa,
anasoma halafu unamsitishia, unamwambia nenda katafute shule nyingine.
"Na ni kweli wana tabia hiyo. “Nina kijana wangu yuko ‘Form One’ (Kidato
cha Kwanza) anasoma shule ... (anataja eneo ilipo shule hiyo), yaani
anasoma kupindukia. Nilikuwa na wasiwasi hata akija likizo hawezi kula
vizuri, anasoma tu."
Alisema kuwa katika shule hiyo ya jijini Dar es Salaam anayosoma mtoto
wake, wameambiwa ni lazima awe na wastani wa kuanzia alama 50 katika
mitihani ya shule ili aruhusiwe kuingia kidato kinachofuata, vinginevyo
wakatafute shule nyingine.
"Katika utaratibu wa elimu, siyo sahihi kufanya hivyo, wewe kama
wanafunzi wameshindwa, wewe siyo ndiyo mwalimu, ndiyo kazi yako ya
kufanya wanafunzi waelewe," alisema na kufafanua zaidi:
“Sasa ukiwa unafanya hivyo, mwisho wa siku utakuwa unafelisha darasa
zima na kujitamba kwamba unafaulisha kwa sababu umefukuza wengi na
kubaki na wazuri wachache. Sasa hiyo ni biashara, siyo elimu tena. Wewe
kama ni mwalimu, unatakiwa kufundisha wanafunzi wote.
“Kwa hiyo, wanasema shule za ‘private’ (binafsi) zinafaulisha wanafunzi
wote, kumbe wengine mliowachuja. Mimi binafsi sikubaliani na hali hiyo
kabisa."
Alisema ni muhimu wizara yenye dhamana ya elimu nchini iweke masharti
kwamba ukishadahili wanafunzi, wasiondolewe shuleni kwa utaratibu wa
viwango vya ufaulu katika mitihani ya shule husika isipokuwa kwa sababu
za tabia mbaya na zisizofaa kwa mwanafunzi kwa mujibu wa sheria za nchi.
MAKUNDI YA UELEWA
Msomi huyo alisema wanafunzi wamegawanyika katika madaraja mawili
kiuelewa darasani, la kwanza likiwa la wenye uelewa wa haraka (fast
learners) na jingine likiwa la wenye uelewa hafifu (‘slow learners).
"Wote hao wanapaswa wazingatiwe katika elimu. Sasa hawa (shule binafsi)
wenyewe wanaangalia 'fast learners' tu. Ni vema wote wakachukuliwa
katika vigezo sawa, siyo unawachuja wengine halafu unasema unafaulisha
wote," alisema Prof. Mushi.
BIASHARA
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba, akizungumza na
Nipashe jana kuhusu changamoto hiyo, alisema si vyema kumfukuza,
kumkaririsha darasa au kumhamisha mwanafunzi aliyefanya vibaya katika
mitihani ya shule.
"Mtihani wa Kidato cha Pili ni mchujo sahihi tu. Shule binafsi
wanakosea. Ufundishaji wa kawaida huwezi kuwa na wanafunzi wanaopata
daraja la kwanza na la pili tu," alisema.
"Hao shule binafsi kuna muda wanateleza kidogo, kwa sababu hakuna
mwanafunzi asiyefundishika labda kwa sababu wao wanataka suala la
biashara. Ni kuonea wanafunzi, bahati mbaya akishaanza shule ya
'private' (binafsi) kidato cha kwanza, hawezi kurudi kwenye mfumo wa
serikali, kwa hiyo wanafunzi wanahangaika," alisema zaidi Mukoba.
Saturday, 24 December 2016
Saturday, 17 December 2016
Bunge la Israel laondoa sheria ya sketi fupi
Bunge la Israeli limetupilia mbali
sheria za kuvaa kwa wafanyakazi wa bunge baada ya wafanyakazi hao
kupinga sheria zinazowataka kutovalia sketi fupi.
Wafanyajazi hao walidai kuwa walinzi katika bunge walikuwa wakitekeleza sheria hizo na kuwazuia watu kuingia bunge hilo.Spika Yuli Edelstein alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa baada ya malalamiko kuhusu mavazi yasiyoridhisha.
Sasa timu itateuliwa kuangalia vile sheria hizo zitatatekelezwa.
Mwezi Oktoba usimamizi wa bunge ulituma barua kuwakumbusha wafanyakazi wote wa bunge kuhusu sheria hiyo ya mavazi.
Tuesday, 13 December 2016
MZEE WA UPAKO AWAOMBEA KIFO.....
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako amesema waandishi wote wanaoandika habari za kumchafua watakufa kabla ya kufika Machi mwakani.
Kauli hiyo aliitoa jana ikiwa ni mwendelezo wa mahubiri yake ya nne katika wiki ya tatu mfululizo, akijibu yaliyoandikwa kwenye vyombo vya habari kuhusu kumfanyia fujo jirani yake na kulewa.
“Kila mwandishi aliyeniandika vibaya ikifika mwezi wa tatu akiwa hai, mimi naacha kuhubiri, nafunga virago nakwenda kuuza gongo, sasa Mungu ndiye ataamua kwamba ama niache kuhubiri mimi au wewe ufe …najua hata leo mpo humu mmekuja na mnasikiliza tu,” alisema.
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako jana amesema waandishi wote wa habari wanaoandika habari za kumchafua, watakufa kabla ya kufika Machi 2017.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni mwendelezo wa mahubiri yake ya nne katika wiki ya tatu mfululizo, akijibu yale yaliyoandikwa katika vyombo vya habari kuhusu kumfanyia fujo jirani yake na kulewa.
“Kila mwandishi aliyeniandika vibaya, ikifika mwezi wa tatu akiwa hai, mimi naacha kuhubiri, nafunga virago nakwenda kuuza gongo, sasa Mungu ndiye ataamua kwamba ama niache kuhubiri mimi au wewe ufe …najua hata leo mko humu mmekuja na mnasikiliza tu,”alisema.
“Akisema Mungu uishi wewe basi, nakuwa sina namna, lakini sijawahi kumtumikia Mungu ambaye ananyamaza. Nilishakubaliana mimi na Mungu, mpango wa Mungu ndiyo mpango wangu, sasa wajiandae, mimi siyo Sheikh Yahaya, mmeingia choo cha kike, nasema ‘Mama yangu mzazi’ nitaacha kuhubiri, nitaacha kuhubiri ….mimi nina nguvu saaana,”alisema.
Hata hivyo baadaye mchungaji huo alishuka na kusema anamuachia Mungu wake ambaye atawahukumu kwa wakati wake.
“Lakini Mungu anasema tusihukumu, namuachia Mungu atawahukumu kwa wakati wake, haleluya, haleluya, Mungu awabariki sana."
Novemba 24, mitandao ya kijamii ilikuwa na picha zinazomuonyesha Mzee wa Upako akirushiana maneno makali na jirani huyo ambaye anasikika sauti.
Taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kiroho zilisambaa baada ya mwandishi wa habari, Happiness Katabazi aliyeshuhudia tukio hilo, kuandika kwa urefu kisa hicho na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Novemba 26, Mzee wa Upako kwa mara ya kwanza alisita kuzungumzia sakata hilo na badala yake akasema wanaomtuhumu waendelee kusema: “Sisemi, lakini siogopi kwenda jela mimi na kwa taarifa yao watashindana sana, lakini hawatashinda. Hii ni kama kumpiga chura teke.”
Novemba 28, pia Mchungaji huyo akajibu akisema maneno aliyotumia ambayo ni mshenzi, mpumbavu na mjinga siyo matusi kwani yameandikwa kwenye biblia na kwamba watu hao ndiyo walianza kumtukana yeye baada ya kuwauliza wanatafuta nini eneo la getini kwake.
Jana, mchungaji huyo aliwahakikishia waumini wake akisema waandishi walioandika kwa lengo la kumchafua watakufa kabla ya kufika Machi mwakani.
Katika mahubiri yake yaliyojengwa na msingi wa Biblia kutoka kitabu cha Samweli wa kwanza, sura ya 16, mstari wa saba, Mzee wa Upako aliyekaribishwa kwa nyimbo kadhaa ikiwamo ‘kusanya kusanya’ alisema yeye siyo mchungaji anayejikweza, lakini baadhi ya wachungaji wakubwa kutoka nje wamekuwa wakienda kuomba upako.
Pia, alisema hata Rais John Magufuli hakumuita yeye bali aliona kitu ndani yake na kubarikiwa kabla ya kumtembelea.